"Fahari ya Utu Wetu"

Breaking

Tuesday 11 July 2023

VIONGOZI WA DINI WAPONGEZA SERIKALI KWA KUTEKELEZA MRADI WA KUZALISHA UMEME

Na Timotheo Mathayo, Rufiji Pwani.

Viongozi wa Dini wameipongeza Serikali kwa usimamizi wa Mradi wa kimkakati wa  kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha megawati 2,115 kuanzia Juni, Mwaka 2024, baada ya ujenzi wake kukamilika.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ziara ya Viongozi wa Dini kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Viongozi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) waliotembelea mradi huo Jumanne Julai 11, 2023.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Askofu Lazarus Vitalis Msimbe kutoka Jimbo Katoliki la Morogoro amesema kuwa wanaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa Mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere.

 “Tunaipongeza Serikali kwa kuthamini nafasi ya Viongozi wa dini hasa katika shughuli za maendeleo na kuamua kutoa fursa ili tuweze kuja kutembelea Mradi wa kimkakati wa Julius Nyerere ambao umefikia hatua nzuri ya utekelezaji," ”amesema Askofu Msimbe.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Maimbo Mndolwa kutoka Umoja wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) amesema kuwa wataendelea kuhamasisha waumini wao ili waweze kutunza mazingira kwa manufaa ya Taifa ikiwemo Mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere.

“Ukipita katika Vijiji vingi vilivyokuwa giza hivi sasa kuna nuru na nuru hiyo ambayo watu wengi walikuwa wakiitafuta mjini kwa sasa ipo hadi vijijini, jambo ambalo limechochea ukuaji wa maendeleo na kuwafanya vijana kubaki vijijini,” amesema Askofu Maimbo.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba amewapongeza viongozi hao kwa kutembelea Mradi wa kimkakati wa Julius Nyerere ambao umefikia asilimia 90  ya utekelezaji wake.

Kina cha maji katika Bwawa kimefikia mita 163.7 kutoka usawa wa bahari na kina cha juu ni mita 184 na kina cha chini kabisa ili kuweza kuzalisha umeme ni mita 163 kutoka usawa wa Bahari.

“Kwa ujazo wa maji uliopo katika Bwawa la Julius Nyerere unatosha kuanza kuzalisha umeme kama kazi ya kufunga mitambo inayoendelea ingekuwa imekamilika pamoja na nyumba ya kuzalisha umeme ambayo imefikia asilimia 70," amesema waziri Makamba.

"Matarajio ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo February, 2024 tutaanza kufanya majaribio ya kuzungusha mitambo ya kuzalisha umeme na ifikapo mwezi Juni, 2024 umeme wa kwanza utaingizwa kwenye gridi ya Taifa,” amesema waziri Makamba.

Ziara hiyo imehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga na Watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la umeme Tanzania (TANESCO).
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba (wa tatu kutoka kushoto) akiwa na Viongozi wa Dini wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya Mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) iliyofanyika Julai 11, 2023 Rufiji katika mkoa wa Pwani.
Viongozi wa Dini kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Viongozi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) wakisikiliza maelezo ya maendeleo ya mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere kabla ya kutembelea maeneo mbalimbali ya ujenzi wa mradi huo.
Viongozi wa Dini kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Viongozi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) wakiwa na Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba wakimsikiliza Msimamizi wa Mradi, walipotembelea mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere.
Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba (wa nne kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (wa kwanza kushoto) wakiwa na Viongozi wa Dini wakati wa ziara ya kutembelea Mradi wa kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere iliyohusisha viongozi hao.

No comments:

Post a Comment