"Fahari ya Utu Wetu"

Breaking

Wednesday 16 August 2023

WIZARA YA MAJI YAWASILISHA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA UTUNZAJI VYANZO VYA MAJI

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewasilisha taarifa kuhusu usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira. 
Waziri Aweso ameeleza masuala mbalimbali mtambuka ikiwemo namna Wizara ya Maji inavyotekeleza maagizo mbalimbali ya serikali ikiwemo Kampeni ya upandaji miti rafiki wa maji iliyozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango jijini Mbeya Novemba 2022.
Amesema jumla ya miti 2,541,803 rafiki wa maji imepandwa sehemu mbalimbali nchini katika vyanzo vya maji na kwamba kampeni hiyo inaendelea ili kuhakikisha kila eneo lenye chanzo cha maji linawekewa mazingira rafiki ya kuliwezesha kutunza na kuzalisha rasilimali maji kwa uendelevu.

Kuhusu tathmini ya mazingira  amesema Bodi za Maji za Mabonde sita kati ya tisa zimekamilisha tathimini ya kimkakati ya mazingira na Kijamii (SESA) ya Mipango shirikishi na mabonde saba yakikamilisha kazi ya mapitio ya mipango shirikishi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji.

Eneo lingine lililofanyiwa kazi ili kuhakikisha Watanzania wanaendelea kunufaika na rasilimali maji ni kuanzishwa kwa kamati 17 za vidaka maji ambazo zinafanya kazi katika mabonde sita ya maji nchini. Mhe. Aweso amefafanua kuwa kamati hizi zimekasimiwa baadhi ya majukumu ya Bodi za Maji ili kurahisisha usimamizi wa rasilimali maji katika eneo husika. 

Aweso amesema katika maeneo ya maji shirikishi Wizara ya Maji imeendelea kusimamia makubaliano ya kimataifa ili kuhakikisha ushirikiano huo unalindwa na kuifanya Tanzania kuwa salama katika matumizi ya maji. Hatua hii imewezesha kujengwa kwa vituo Nane vya kisasa vya kukusanya takwimu za mtiririko wa maji katika mito mikubwa ya Mara, Kagera, Simiyu na Rusumo iliyoko Bonde la Maji la Ziwa Victoria.
Mhe. Aweso amesema Wizara ya Maji imejifunza na kupata majawabu kupitia matukio mbalimbali ikiwemo tukio la ukame lililotokea miaka ya hivi karibuni na kusabisha baadhi ya mito kuwa na upungufu wa maji. 

“Hatutaki na hatutegemei haya yajirudie tena siku nyingine.”  Mhe. Aweso amesema.

Wajumbe wa Kamati hiyo wamepongeza na wameishukuru Wizara ya Maji kwa utayari wake wa kuhakikisha maagizo mbalimbali yanayotolewa na viongozi yanatekelezwa. Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) amesisitiza na kuitaka wizara ihakikishe inaendelea kusimamia utekelezaji wa maagizo ya viongozi kwani maji ni rasilimali muhimu ambayo haina mbadala. 

No comments:

Post a Comment